MCHEZO WA NG’OMBE
Imeandikwa na ABDULLAH AMUR SULEIMAN
Ingawa kumcheza ngo’mbe ni mchezo ambao wenye kuhusika nchi kama Ureno, Spain, Brazil na nchi nyingine za Latin America, Mchezo huu huchezwa hapa Tanzania katika kisiwa cha Pemba.
Wareno kwa miaka mingi walitawala Bara hindi na hivi tu karibuni walitolewa katika ile sehemu yao ya Goa iliyomo katika nchi ya Bara Hindi. Serikali ya Bara Hindi iliona aibu kuwa sehemu yake bado inatawaliwa na dola ya kigeni.
Utawala wa Kireno katika sehemu hii ulileta maafa makubwa sana na mtu asikiapo hizo hadithi za ukatili ambazo wareno wakizifanya basi atawaoneya huruma wale ndugu zetu kama wa Msumbiji, Angela na Guinea Bissau ambao bado wanatawaliwa na Wareno.
Katika karne ya kumi na tatu na kumi na nne pamoja na kuendela mbele, dola ya Kireno ilikuwa dola kubwa ya kuhishimika na kutowa wasafiri mahodari kama Vasco da Gama, Columbus na wengineo. Hawa walihatarisha maisha yao kwa ajili ya kupata utajiri, kuweza kuuza bidhaa zao na kukamata watu wanyonge na kuwauza kama watumwa.
Ingawa kuna mengi ambayo yanatafautiana na namna ya ng’ombe achezavyo kama vile hakuna kizazi maalum ambacho ng’ombe wakali wanahusika nacho bali ng’ombe yo yote dume huwa mwenye kufaa kwa mchezo huo bila ya wasiwasi wo wote.
Hakuna taaluma au mazowezi ya mwanzo kwa kuwafanya ng’ombe dume kuwa wanaufahamu mchezo huu. Watoto wadogo wa huko Pemba wakiwa wanaume, huwachiwa mifugo kuipeleka malishoni na kuwatazama wasiharibu mimeya ya watu katika mashamba yao.
Watoto hawa kwa vile kukaa tu na kutazama ng’ombe wakila majini kutwa ni jambo lisilowaletea haraka yo yote na hujiona wavivu, kwa ajili ya kuondoa hali hiyo ya uvivu basi huaanza kuwachokoza ng’ombe na namna hii mazowezi ya mchezo huo huaanza kwa wote wawili.
Wavulana hawa humcheza ndama kwanza na kumtania huyo ndama hugungwa kamba ndefu ili asiweze kushambulia kwa ukali na afanyapo hivyo, ile kamba ndefu hukamatwa na kuvutwa nyuma au kuzuwiliwa na hapo hapo mnyama husika kushabulia.
Mchezo wa ng’ombe ni mchezo wa taifa huko Pemba, hapana mtoto wa kiume hata mmoja wa Kipemba, akiwa mwenye asili ya Kiafrika au Kiarabu ambaye hajuwi kumcheza Ng’ombe.
Mchezo huu jinsi unavyopendwa na vijana wa kiume wa Pemba ni kama vile wavulana wanavyoupenda mchezo wa mpira yaani ‘football’, huko Zanzibar, Tanzania bara na kwingineko ulimwenguni.
Aghlabu mchezo wa ng’ombe huchezwa wakati wa watu ambao wamerejea mavunoni na karafuu zimekwisha tena na hapo hutazamiya kustarehe. Watu wengi hujumuika kwenye sherehe hizo za mchezo wa ng’ombe na hawaji tu kuona mchezo huo lakini hulipa ada maalum kwa ajili ya kuuona namna mchezo huo ufanywavyo na mastadi wake hodari.
Kabla ya mchezo kuwepo, hujengwa bigili kubwa na pembezoni hujengwa bigili jingine dogo. Hili bigili kubwa huwa kwa ajili ya kupatikana kwa uwanja au nafasi ya mchezo huo kufanywa. Lele dogo huwa kwa ajili ya wapiga ngoma na wanawake waimbao kwa kusherehekeya mchezo huo.
Siku moja kabla ya mchezo huo kuwa tayari, ng’ombe ambao wanachezwa, hushindishwa kwa njaa kwa muda wa saa 24 au zaidi. Ng’ombe kama hao huwa wanaelewa na mchezo wa ng’ombe na kwa vile muda mkubwa hawakupata riziki yo yote huwa wakali kikweli.
Kutolewa kule walikofungwa na kuletwa kiwanjani, wakiwa wanatiwa ndani ya bigili jingine dogo na mchezo ukiwa tayari huenda watu wakawachukiwa mmoja mmoja na kumleta kiwanjani na kuchezwa kwa muda Fulani na baadaye kurejeshwa.
Kuna hatari ya mtu kupoteza maisha yake au kujeruhiwa na huyo ng’ombe ambaye anachezwa kwa hivyo ule ng’ombe huwa na tundu puani ambayo kamba au shemere hupitishwa na baadaye kamba ndefu hufungwa na hiyo shemere. Makusudio ya kufanya hivi ni lile gombe wakati linapohemkwa basi watu hukamata hiyo kambao ndefu kwa hodar na kumfanya ng’ombe asihiliki binaadamu.
Katika nchi za Ureno, Spain, Barazil na nyinginezo za Latin American, kuna aina maalum ambazo hutowa ng’ombe wakali. Kinyume cha Pemba, huko kwenye nchi hizo, ng’ombe hafungwi shemere bali huwachiliwa akakumbana ana kwa ana na yule anayemcheza. Wawili wao tu huwa uwanjani.
Huko Pemba, kuna ulalamishi mkubwa kwani ng’ombe hachezwi na mtu mmoja bali watu wapatao sita hadi kumi huwa wanamcheza ng’ombe mmoja. Kwa namna hii yule nyama hubabaika na asijuwe wa kupambana naye ana kwa ana ni nani.
Juu ya hivyo katika mbabaiko huu, ng’ombe huweza kukabiliana na wachezaji na kuwashambulia. Wachezaji huwa wameshika kitambaa, shuka au kipande cha mkeka ili akija ng’ombe wamgubike nacho usoni na yeye yule mnyama asiweze kumuona yule aliyemgubika kwa hivyo hupigwa ngeya au chenga.
Mtu mwenye kujusurisha na kumkabili ng’ombe na kumpiga ngenya nyingi, huwa ndiye mwenye kustahiki ushindi na sifa katika mchezo huu na hupewa zawadi maalum kama kanzu nzuri ya darizi, kofia ya kazi au mapesa. Isitoshe hushangiliwa sana na watazamaji na wakati apigapo ngeya, hushangiliwa sana na wal e akina mama ambao wamo kwenye bigili wakiimba na ngoma kupigwa wakiongozwa na mpigaji zumari.
Kule Spain, Ureno, Brazil ana nchi nyinginezo za Amerika ya Kusini, aghlabu ng’ombe huuwa au huuliwa kwani hatari huwa hazikadiriki ikiwa ni ng’ombe ndiye alimshinda binaadamu. Na binaadamu akimshinda ng’ombe basi hupewa upanga na visu vidogo vidogo na humchoma huyo ng’ombe hadi akaanguka chini hajiweze na amekufa. Hapo wa hushangilia sana. Ukatili kama huo haupo huko Pemba.
Ng’ombe mmoja akisha chezwa basi huletwa mwingine na akachezwa uwanjani. Hawa ng’ombe hukodiwa kwa wenyewe na wale wawachezao vile vile hukodiwa wa ujira Fulani. Watu au mtu Fulani hujikakamua na kuufanya mchezo huu kwa gharama zake au zao. Hupata faid kama mchezo umehudhuriwa na watu wengi la mahuhudhurio yakiwa kidogo hasi huenda mumbi au hupata hasara.
Ng’ombe hawa wanchezwa na hasa wale waliokuwa wakali aghlabu huandamishwa na shetani na huwa mkali kweli. Kabla ya kwenda mchezoni, hufanyiwa ya kufanyiwa na pengine huvikwa hirizi usoni mwake au kufungwa nayo miguuni mwake. Mchezo unapomalizika basi mafundi au waganga huwatowa hao mashetani na wanyama maisha yao huwa kama desturi.
